Sunday, April 19, 2015

NCHI ZA AFRIKA ZA TOA MSIMAMO WAO KWA IMF NA WB

Waziri wa Fedha Mhe. Saada Salum Mkuya akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile kushoto kwake kwa pamoja wakifuatilia kwa makini mkutano wa 10 wa kisheria wa kundi la Afrika (Afrikca Group Constituency) uliokuwa ukiendelea mjini Washington DC.ha3Waziri wa Fedha Mhe. Saada Salum Mkuya akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile kushoto kwake kwa pamoja wakifuatilia kwa makini mkutano wa 10 wa kisheria wa kundi la Afrika (Afrikca Group Constituency) uliokuwa ukiendelea mjini Washington DC.
Akizungumza na vyombo vya habari,waziri wa fedha wa Tanzania Mhe. Saada Salum Mkuya alisema” Sisi kama nchi tuliwasilisha nini tunaona katika utekelezaji wa mipango ya Benki. Tumeshukuru sana Benki ya Dunia kwa kuendeleza mipango ya kuweza kusaidia nchi za kiafrika ,hususan kwenye mipango ya kujenga miundo mbinu ya kiuchumi kama vile barabara, kilimo pamoja na miundo mbinu ya maji na umeme”.
“Lakini vilevile tumeonyesha wasiwasi wetu kutokana na sera ambazo Benki ya Dunia imeziweka, kama vile kuangalia sera zile za watu wa kiasili ya kiafrika, sisi tumehisi mbali ya nia nzuri na njema ya Benki hii ya Dunia, lakini inaweza kuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi zetu kwa sababu sera hiyo inaweza kutumika kuigawa nchi ambayo misingi yake imekuwa ikijengwa kwa umoja kutoka uhuru”.Alisistiza Mkuya.
Hakuishia hapo aliendelea kutoa mfano kuwa “sisi watanzania tumekuwa wamoja ingawa tuna lugha mbalimbali kutokana na makabila tofauti. Lakini tumekuwa pamoja kwa kipindi cha miaka 50.Kwa hiyo tumeona sera hiyo isije ikatumika kwa ajili ya kuwa kigezo cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini . Sisi kama wa Afrika na viongozi wa Afrika tunashirikiana kuona kuwa sera zinazowekwa hazitukwamishi”.
Hali hii ya kudai uasilia (indigenous) imeibuka zaidi katika miongo hii miwili, wakati kukiwa kumejitokeza watu wanaodai kuwa wao hawatambuliki na hoja hii inaihusu hasa nchi ya Tanzania.
Mawaziri wa Fedha kutoka Afrika wamejadili mambo mbali mbali ambapo ni pamoja na masuala ya maendeleo na mahusiano yao na Benki ya Dunia. 
Katika Mkutano huo wa kisheria Mkurugenzi Mtendaji ndiye ambaye amewasilisha maazimio ya Benki katika kipindi cha miezi sita.Aliongeza Mkuya. Aidha katika mkutano huo pia walizungimzia suala la Ebola. “Kwa kweli wamekubali kusaidia nchi zile ambazo zimekumbwa na gonjwa hili lakini wamezitaka nchi za afrika na zenyewe kushirikiana katika kupambana na gonjwa hili”.Alimalizia Mkuya.
Mikutano hiyo bado inaendelea hapa mjini Washington DC. Hali ya hewa ni baridi kiasi.
Imetolewa na Msemaji :Wizara ya fedha
Ingiahedi C.Mduma
Washington DC
18/04/2015

Msama afafanua yanayojiri Kituo cha Honoratha


  Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu taarifa za upotoshwaji zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Honoratha kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu taarifa za upotoshwaji zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Honoratha kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam.

NA LOVENESS BERNARD


MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama, amesikitishwa na taarifa za upotoshaji zilizotolewa hivi karibuni kuhusu kituo cha kulea watoto yatima cha Honoratha kilichopo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Msama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tamasha la Pasaka, amesema kuwa Kituo hicho ni moja ya vituo anavyovihudumia kila mwezi na hakina tatizo la kuwalaza watoto madarasani, kwani wana vyumba kwa ajili ya malazi na kwamba, picha zilizoonyeshwa  zilipigwa watoto hao wakiwa darasani. 


‘’Nimesikitishwa na taarifa hizi, kwani Honoratha ni moja ya vituo ambavyo ninavihudumia, changamoto zao nazifahamu...Kinalea watoto vizuri na baadhi yao wengine tunawasomesha vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini,” alisema Msama.


Aidha, Msama amevitaka vyombo vya habari kuandika habari za ukweli na uhakika ili kuepuka usumbufu  utakaojitokeza kwa wahusika, ikiwamo kwa mlezi na watoto wanaoishi katika kituo hicho ambao walipata adha baada ya taarifa hiyo kutoka.


Alisisitiza kuwa, taarifa hizo hazina ukweli wowote kwani hata mlezi wa kituo hicho hawakufanya mahojiano naye, ikiwamo kumuuliza kwa nini watoto hao walilala darasani mchana huo.


Msama amekuwa akisaidia vituo mbalimbali vya kulea yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kupitia vyanzo vyake mbalimbali ikiwamo mapato yanayotokana na Tamasha la Pasaka.

NYALANDU: UMOJA WETU NDIO UTATUFANYA TUSONGE MBELE

Waziri wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na aliyewahi kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha, Joshua Kileo (Kulia)  baada ya ibada katika kanisa la KKKT Mjini Kati siku ya Jumapili.
************
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema pamoja na mitihani mikubwa ambayo taifa inakabiliana nayo, umoja wa Watanzania utaifanya nchi isonge mbele kama taifa linalozingatia sheria na demokrasia.

Akizungumza baada ya Ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mjini Kati jana, Nyalandu alisema nchi itafanikiwa kupita mitihani hiyo kama wananchi wataimarisha umoja kati yao.

“Nchi inapita huku kukiwa na mambo mengi makubwa kufanya…kila mmoja anahitaji amani na hiyo tunaweza kuipata au kufanikiwa kupita salama iwapo tutakuwa na umoja.

“Nchi yetu itasimama, itashinda mitihani ambayo tunayo kama ya uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu, upigaji wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu,” alisema.

Mapema katika mahubiri yake kanisani, Mteolojia Solomoni Dereva, aliwaomba Watanzania kuliombea taifa kwa Mungu ili liweze kupita kwa utulivu katika kipindi hiki chenye mambo makubwa.

“Tumuombe Mungu pia atuletee viongozi wazuri, wenye sifa ambao watatutoa hapa tulipo na kutufikisha mbele zaidi katika maendeleo,” alisema.

Alisema kiongozi mzuri ni sawa na mchungaji mwema ambaye huanza kuchunga nafsi yake dhidi ya matendo maovu kama rushwa na ubinafsi na pia huchunga familia yake na ofisi aliyokabidhiwa ili kuwatumikia wananchi.

Katika kipindi cha "HUYU NA YULE" kesho (Jumatatu), usikose kujua UNDANI wa maisha ya Linda

Kesho Jumatatu katika kipindi cha huyu na yule cha mahojiano na mwanamitindo mbunifu wa LB kutoka Atlanta, Georgia atakapoelezea historia yake yenye milima na mabonde historia ya maisha yake yenye huzuni na furaha wakati mwingine Linda akitokwa na machozi kwa kukumbuka maisha aliyopitia. Je Mume wake Mali walijuana nae wapi? na mengine mengi kuhusu maisha yake ikiwemo kampuni yake ya LB na malengo yake ya kupeperusha bendera ya Tanzania anga za kimataifa. USIKOSE mahojiano yaliyofanywa na mwakilishi wa Vijimambo na kwanza production Michigan Alpha Igogo ambae alitaka kujua undani wa maisha ya mwanadada Linda

Alpha Igogo akifanya mahojiano na Linda jijini Atlanta
Maswali yalikua moto Linda akipumua na kumkumbatia Alpha Igogo baada ya mahojiano kufikia mwisho

HARAKATI ZA KUANZISHWA KWA KARIAKOO FAMILY FOUNDATION (KFF)

 Mwenyekiti wa Kariakoo Family Foundation (KFF) Mohamed Bhinda akiongoza kikao cha Kamati ya Utendaji katika kuandaa rasimu ya katiba ya chama hicho kinachotarajiwa kusajiliwa  hivi karibuni kama taasisi isiyo ya kiserikali kwa nia ya kukutanisha upya wadau wote waliozaliwa, walioishi na wenye asili ya Kariakoo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam. Mkutano huu umefanyika leo jioni Kinondoni Studio. Kulia kwa Bhinda ni katibu wa chama hicho Senpai Wahid
 Mtunza hazina wa KFF Yahaya Sameja akielezea namna chama hicho cha jamii ya wana Kariakoo kitavyoweza kujiendesha kwa njia za ada, michango na misaada ya wafadhili katika kuendeleza wanachama, ikiwa ni pamoja na kusaidiana katika shida na raha. Kushoto ni Mwenyekiti wa KFF Mohamed Bhinda na kati ni Makamu Mwenyekiti Tatu Lumelezi
 Wana KFF wakipata mlo wa mchana wakati wa mapumziko
Jopo la kamati ya utendaji ya KFF baada ya mkutano wao leo

A New Book By Hamisi Kigwangalla: Kigwanomics and The Tanzania We Want: From Renaissance to Transformation

Ndugu,

Ninafuraha isiyokadirika kwa hatimaye kufanikisha kazi niliyoianza takriban miaka minne iliyopita kuandika kitabu kinachoainisha mawazo yangu juu ya Tanzania tuitakayo, Tanzania ya mabadiliko, Tanzania ya mapinduzi kuelekea kupata maisha bora kwa kila mtu. Ndani yake nimejaribu kuelezea, kwa kadri nilivyojaaliwa, jukumu la kizazi chetu ni nini haswa? 

Misingi ya ukombozi wa kiuchumi na kijamii ni ipi haswa? Nini chanzo cha umaskini na utajiri wa nchi? Nini kifanyike ili tuvune na kufaidika na utajiri tulionao? Nini vipaumbele na mbinu za ukombozi tunaoutaka sana sasa? Ni nini yanapaswa kuwa mabadiliko tunayoyatarajia? 

Katika kitabu hiki naweka mapendekezo ya mfumo mpya wa kuendesha uchumi kwenye nchi zinazoendelea za Afrika kutokana na misingi ya utamaduni asilia wa kiafrika, nazungumzia nguzo nane za mfumo huu, ambao nimeuita 'African Socialism with Capitalist Characteristics'. Kanuni hizi zilizosheheni muundo wa fikra zangu, uliwahi kuitwa 'Kigwanomics' na rafiki yangu Michael L. Wilson (Ph.D.) wakati tukijadili mambo mbali mbali ya kiuchumi na mustakabali wa Africa tunayoitaka akiufananisha na mawazo ya watu wengine mashuhuri duniani waliowahi kusimamia mabadiliko kwenye nchi zao na kufanikiwa, kama Ronald Reagan (Reaganomics) ama Thaksin Shinawatra (Thaksinomics). Nami nilipenda kuazima style hii na kukiita kitabu changu, Kigwanomics.  

Katika kitabu hiki utasoma uchambuzi wa mawazo ya waandishi mashuhuri duniani kama akina Mchumi Prof. Paul Collier (The Bottom Billion n.k.), Dr. Chika Onyeani (The Capitalist Nigger), Why Nations Fail (Drs. Robertson and Acemoglu), What went wrong with Africa (Roel van der Veen), Dead Aid (Dr. Dambisa Moyo), Towards the African Renaissance (Prof. Cheikh Anta Diop) na wasomi wengine wa Africa.  

Imani yangu ni kwamba nimetoa changamoto ya namna mpya ya kufikiria juu ya mapinduzi ya upili (Secondary revolution) kuelekea Tanzania iliyozaliwa upya (Tanzanian Renewal). Lengo kuu la mawazo yangu kwenye kitabu hiki ni hili. Kama ukisoma na ukaona upya wa mawazo yangu, na haja ya kuiunda upya Tanzania Tuitakayo basi nitakuwa nimefanikiwa. 

Kitabu kitazinduliwa rasmi taratibu zitakapokamilika na tutakujulisha. Nimeandika kitabu changu kwa lugha ya kiingereza, na tayari kuna timu, inayoongozwa na Ndg. Prince Bagenda, inafanyia kazi tafsiri ya kiswahili, na kuna wataalamu wanaofanya kazi ya kuandaa 'popular version' ya kitabu hiki kwa lugha ya kiswahili ili kufikisha mawazo haya kwa haraka na kwa watu wengi zaidi. 

Ikikamilika kazi hii ndipo tutatangaza siku, mahala na saa ya kukizindua rasmi. Kwa sasa kinauzwa kwa bei ya 'promotion' ya TZS 5,000 kwa kila nakala, kwenye maduka ya TPH Bookshop na maduka yote ya Uchumi Supermarkets, Mlimani City (MAK Bookshop), pia kipo kwenye mikono ya wamachinga kwenye njia panda zote kubwa za jijini Dar es salaam, kimefika Iringa (Lutengano Investment), Vyuo Vikuu vyote iringa, Dodoma na Mwanza (Pia Kwa Ibrahim Campbell jirani na CRDB Mwanza Branch). 

Nakutakia usomaji mwema. Natanguliza Shukrani zangu za dhati na fanaka. 

Wakatabahu,
Hamisi Kigwangalla.
Mwandishi. 

 
Nafasi Ya Matangazo